Wednesday, October 24, 2012

Mwanamke kuwa chini ya Mwanaume sio sababu ya kunyanyaswa




LIPO jambo gumu katika ulimwengu wa uhusiano ambalo limekuwa tatizo kubwa na fumbo linalowashinda wengi. Nazungumzia mwanamke kuwa chini ya utawala wa mwanaume. Kwa ujumla ni jambo la kawaida kabisa.

Huu ni msingi uliojengwa tangu zamani na hata kwenye mapitio ya vitabu vitakatifu yanaeleza juu ya jambo hilo. Kimsingi, hakuna tatizo katika nguvu hiyo ya mwanaume. Katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia, mambo yamebadilika kidogo na angalau mwanamke anapata nafasi mbalimbali kwenye jamii.

Wanawake wa leo wanapewa vipaumbe kwenye uongozi wa makampuni, taasisi, madhehebu ya dini, mashirika na vyama vya siasa na serikali. Pamoja na yote hayo, bado mwanamke anabaki kuwa mwenye wakati mgumu sana katika kufanya uamuzi au kujua hatma yake akiwa kwenye lindi la mapenzi.

Anaweza kuwa mwanamke bora, mwenye msimamo na tija kazini, lakini kwa mpenzi/mumewe anakuwa mpole asiyejua chochote kitakachokuwa mbele yake.

Ni eneo ambalo mwanamke anakuwa hana ujanja, hajiwezi na hajui cha kufanya, kwa sababu kila kitu kinachohusu uhusiano kwake kinakuwa na giza nene mbele yake. Huu ni ukweli.

Ni mada yenye ugumu kidogo kuingia akilini, lakini kichwa kikitulia na kupitia kwa umakini mkubwa, mstari kwa mstari unaweza kuelewa vyema na kubaki na kitu kipya kichwani mwako.
 
NI NINI HASA?
Ni kuwa chini ya mamlaka ya mwanaume. Kuwa chini ya matakwa na kufuata maelekezo. Wakati mwingine anaweza kupata nafasi ya kutoa mawazo yake, lakini ni juu ya maisha tu – si mustakabali wa mapenzi yao.

Mwanamke anaweza pia kutoa mapendekezo ya mapenzi yao, lakini hayawezi kuwa uamuzi. Hata kama akitoa uamuzi, bado siri ya uhusiano huo inabaki kuwa ya mwanaume. Mwanamke anaweza kuwa na upendo mkubwa, lakini akitegemea zaidi sapoti ya mwanaume wake.
Kwa maneno mengine, hata kama ana mapenzi yenye ukubwa gani, kama mwanaume wake atakuwa na uamuzi mwingine ambao yeye haujui, yote yanaweza kuwa kazi bure mwisho wa siku.
 
NI SAHIHI?
Hakika. Hakuna tatizo kwa mwanaume kuwa na mamlaka au uamuzi juu ya uhusiano wake. Si kwamba yeye ndiye aliyejipangia mwenyewe bali ni utaratibu alioukuta baada ya yeye kuzaliwa.
Mwanaume aliumbwa na kukabidhiiwa mamlaka moja kwa moja (mapitio ya vitabu Vitakatifu yanathibitisha hilo).   
 
KUNA ATHARI?
Ndiyo! Hapa ndipo kwenye msingi hasa wa mada yetu. Rafiki zangu, mamlaka ya mwanaume yamekuwa machozi kwa wanawake wengi. Kwa sababu wanawake hawana uwezo wa kujua kilichopo (hasa) ndani ya moyo wa mwanaume, wamekuwa wakitumia mawazo na fikra tu.
Mwanamke anaweza kuupumzisha moyo wake kwa mwanaume lakini akiwa hana uhakika wa nini kinachofuata, wakati mwanaume anaweza kumpenda mwanamke na kuendelea kubaki na siri yake ya nini kinachofuata ndani ya moyo wake.

Tunaona mengi kila siku kwenye jamii yetu. Mwanamke anafanya jambo kwa msingi wa kumfurahisha mpenzi wake, akiwa ameweka athari/mateso ambayo anaweza kuyapata kwa furaha ya muda kwa mpenzi wake.

Hata hivyo kipo kitu cha kufanya rafiki zangu. Kuwa chini ya himaya ya mwanaume hakukunyimi haki ya KUTAMBUA THAMA NI YAKO na NGUVU YA KUFIKIRI ILIYO NDANI YAKO. Bado mwanamke anaweza kuendelea kuwa mwenye mipango na kuamini kwamba nguvu ya ubongo wake ni kubwa kuliko hata mpenzi wake.

Kipo kitu cha kufanya, lakini ili kukufanya uelewe vizuri zaidi mada yenyewe, hebu twende tukaone matatizo wanayokutana nayo wanawake kutokana na kuacha nguvu ya MAMLAKA ya mwanaume ifanye kazi na kushindwa kutumia uwezo wa KUFIKIRI  uliopo ndani yao.
 
SUALA LA MIMBA
Kupata mimba kabla au nje ya ndoa ni tatizo. Ni jambo moja linalowahusu watu wawili lakini likiwa ndani ya uamuzi wa mwanamke. Mimba si bahati mbaya. Wanawake wanajua hili vizuri sana.
Wakati mwingine, wapenzi wanaweza kuwa wamepima ukimwi na hivyo wana uhuru wa kuamua kukutana kwa kutumia kinga au lah, lakini bado kuna suala la mimba ambalo linaweza kumgharimu mwanamke huyo.

Ukiacha hilo, inatokea mwanaume anamlazimisha mwanamke abebe mimba kwanza (eti) ndiyo atapeleka barua ya posa kwao. Inawezekana mwanaume huyo ana lengo hilo, lakini kwa nini alazimishe iwe kabla ya ndoa?

Kwa sababu sasa wanawake wengi huwa wanaacha nguvu yao ya kufikiri, wanajikuta wameingia mkenge! Mwisho jamaa anaingia mitini, mwanamke anabaki na mtoto wake.
Kwa nini uache hili litokee? Kwani hujui namna ya kujikinga na mimba? Ukiachana na kinga, kuna hata njia rahisi ya kuhesabu mzunguko wa mwezi, pia hujui? Nafasi yangu kwa leo imeisha. Hadi wiki ijayo kwa mwendelezo wake.
 
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani

Habari hii ni kwa hisani ya mtandao wa Global Publishers

No comments: